Top Stories

BAYERN MUNICH 6-1 LEIPZIG: LUIS DIAZ APIGA HAT-TRICK

Dakika 12 pekee zilitosha kwa Luis Díaz kuvunja ngome ya RB Leipzig na kuanzisha usiku ambao Bayern Munich iligeuza uwanja wake kuwa sehemu ya kipigo. Kuanzia hapo, wenyeji walitawala mchezo huku wageni wakishindwa kuendana na kasi yao.


Leipzig waliingia uwanjani wakiwa na matumaini ya kuvuruga mipango ya Bayern, lakini walijikuta wakikabiliana na timu iliyokuwa ikisogeza mpira kwa kasi kubwa. Alexander Pavlović aliongeza bao la pili dakika ya 26, kabla ya Michael Olise kufunga la tatu dakika ya 34. Bayern ilienda mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao matatu, huku Leipzig wakionekana kushindwa kupata majibu ya kuzuia mashambulizi ya wenyeji.


Díaz atawala mwanzo, katikati na mwisho


Hat-trick ya Luis Díaz haikuwa bahati ya siku. Alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 12, akarudia kufanya hivyo dakika ya 47 mara baada ya kipindi cha pili kuanza, kisha akakamilisha hat-trick yake dakika ya 69. Kila bao lilikuja katika hatua tofauti za mchezo, huku Leipzig wakizidi kupata wakati mgumu kadiri dakika zilivyokuwa zikisonga.

Ubora wa Díaz ulionekana zaidi ndani ya kikosi chenye washambuliaji wengi wenye uwezo wa kuamua matokeo. Bayern ina wachezaji wanaoweza kuiba nafasi ya kuwa nyota wa mchezo wowote, lakini safari hii Díaz ndiye aliyechukua jukumu hilo.


Harry Kane azidi kuweka rekodi Bundasiriga

Harry Kane, aliweka jina lake kwenye orodha ya wafungaji. Alipachika bao dakika ya 52, dakika chache tu baada ya Díaz kufungua kipindi cha pili kwa bao lake la pili. Mabao hayo mawili yaliyofungwa ndani ya dakika tano yalizima kabisa matumaini ya Leipzig ya kurejea kwenye mchezo.


Zaidi ya bao lake katika ushindi huo, Kane amefikisha michezo 100 akiwa na Bayern Munich, akikusanya mabao 102 na kutoa assist 28. Takwimu hizo zinaonyesha mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Bayern na uwezo wake wa kuendelea kuwa tishio kwa wapinzani.


Leipzig wapambana, lakini Bayern ni darasa jingine


RB Leipzig walijitahidi kupambana katika maeneo waliyoweza. Walikaba kwa nguvu na kushinda mapambano mengi ya mpira dhidi ya wenyeji. Hata hivyo, tatizo kubwa lilikuwa muda mwingi walioutumia bila mpira, jambo lililowafanya washindwe kuzuia mashambulizi ya Bayern.


Mlinda mlango wa Leipzig alikuwa na kazi kubwa zaidi, kwa sehemu kubwa akisakamwa na mashambulizi makali akiruhusu bao sita.


Maksimović aliifungia Leipzig bao la kufutia machozi dakika ya 90+1, wakati Bayern ikiwa tayari imepunguza kasi ya mchezo. Bao hilo lilipunguza tofauti ya mabao kwenye ubao wa matokeo, lakini halikubadilisha simulizi ya pambano ambalo Bayern ilikuwa imelidhibiti kwa kiasi kikubwa.


Ujumbe mzito kwa Bundesliga

Bayern Munich ilitengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga, huku Leipzig wakikikwama kutekeleza mpango wao. Hapo ndipo tofauti ya timu hizo mbili ilipoonekana wazi. Wafungaji wanne tofauti walitikisa nyavu, ishara kwamba hatari ya Bayern haitokani na mchezaji mmoja pekee.


Kwa RB Leipzig, matokeo haya ni somo la gharama kubwa kuhusu hatari ya kuiruhusu Bayern kupata nafasi ya kutawala mchezo mapema. Kwa upande wa Bayern, ushindi huu umeonyesha nguvu ya safu yake ya ushambuliaji, huku Luis Díaz akipiga hat-trick na Harry Kane akiendelea kuthibitisha umuhimu wake kupitia mabao na assist zake.

Comments