- Get link
- X
- Other Apps
Top Stories
- Get link
- X
- Other Apps
Afisa Habari wa Young Africans SC, Ali Kamwe, amezungumzia maandalizi ya Yanga kuelekea mchezo wa CAF Champions League, hali ya kikosi baada ya Kariakoo Derby na hatua iliyofikiwa kuhusu Israel Patrick Mwenda.
Yanga inaingia katika maandalizi ya mchezo huo baada ya kufungwa mabao 2-1 na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, Kamwe amesisitiza umuhimu wa kujiandaa kwa umakini dhidi ya CFFA ya Madagascar, akionya kuwa Yanga haipaswi kutegemea jina lake kupata ushindi.
Ameeleza kuwa Yanga inapaswa kuichukulia mechi hiyo kwa uzito na kuzingatia maandalizi ya mpinzani wake.
"Hatupaswi kuingia katika mchezo huu tukiwa na mawazo kwamba tutapata ushindi kwa sababu tu tunaitwa Young Africans,"
Kamwe amesema wapinzani hujiandaa kutafuta udhaifu wa timu nyingine ili kupata matokeo, hivyo Yanga inapaswa kuwa makini. Timu kutoka Madagascar zimeonyesha ushindani katika mashindano ya soka barani Afrika.
"Hakuna mchezo ambao tunaweza kuuchukulia kirahisi. Tunapaswa kucheza kwa nguvu, kwa ari na kwa kuelewa umuhimu wa matokeo tunayoyahitaji," Kamwe.
Kuhusu hali ya kikosi, Duke Abuya aliumia katika mchezo dhidi ya Simba. Jeraha hilo lingeweza kuonekana la kawaida la mchezo wa soka, lakini limeendelea kumsababishia maumivu na anaendelea kufanyiwa vipimo zaidi. Ripoti ya awali ya daktari inaonyesha anaweza kukaa nje kwa wiki mbili hadi tatu, huku hali yake ikifuatiliwa. Wachezaji wengine wako katika hali nzuri kwa ujumla.
Kamwe pia amefafanua hatua iliyochukuliwa kuhusu Israel Patrick Mwenda. Amesema suala la mchezaji huyo liliwasilishwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, ambayo ilikaa, ikalipitia na kutoa uamuzi.
Mwenda ameelekezwa kurejea kazini na kutii adhabu pamoja na maelekezo ya kamati. Anatarajiwa kurejea mazoezini na kuendelea kuitumikia klabu.
Katika Ligi Kuu ya NBC, Yanga bado ina michezo 23 iliyosalia, hivyo nafasi ya kuwania ubingwa ipo. Kamwe amewaomba mashabiki kuendelea kuwa pamoja na timu.
"Huu si wakati wa kukata tamaa, bali ni wakati wa kuonesha umoja, mshikamano na imani katika klabu yetu," alisema.
CFFA inatarajiwa kuwasili Tanzania leo, Jumanne, kwa ndege ya saa 11 jioni. Ingawa mchezo wa Jumamosi ni wa nyumbani kwa CFFA, michezo yote miwili ya hatua hii itachezwa Tanzania.
Yanga na CFFA zitakutana Jumamosi, 17 Oktoba, saa 9:00 alasiri, katika Azam Complex. Viingilio vitatangazwa rasmi baada ya mkutano na wanahabari, huku klabu ikisema itahakikisha bei zinakuwa rafiki kwa mashabiki.



Comments
Post a Comment