Top Stories

SIMBA IMEJIPATA? AZAM FC 0-2 SIMBA SC

Simba SC bao lao leoAzam FC  0-2 Simba SC 

Simba Sports Club imeichapa Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ikiendelea na mwanzo wake wa msimu bila kupoteza mchezo baada ya kufikisha ushindi wa sita mfululizo.

Ushindi huo unaacha swali moja kubwa: je, Simba imejipata? Picha inayoonekana katika michezo yake ya hivi karibuni ni ya timu inayozidi kuelewana, kucheza kwa pamoja na kutumia zaidi mfumo kuliko kutegemea mchezaji mmoja kuibeba timu. Chini ya Steve Barker, hilo limeanza kuonekana katika namna wachezaji wanavyobadilishana nafasi na kujenga mashambulizi.

Dhidi ya Azam, Simba haikulazimisha njia moja ya kufika kwenye lango. Mashambulizi mengi yalijengwa kutoka pembeni, kisha mpira kuletwa katikati kwenye maeneo ambayo yanaweza kuleta madhara. Mbinu hiyo iliipa Simba njia tofauti za kuishambulia Azam na hatimaye kuzaa matokeo katika kipindi cha pili. Licha ya Azam FC kichezea vizuri katika kIpindi Cha kwanza.

Simba SC bao lao leo

Bao la kwanza lilifungawa dakika ya 59 na Rushine De Reuck, ambae pia ametwaa tuzo ya mchezaji Bora wa mchezo wa leo kabla ya Clatous Chama kuongeza la pili dakika ya 68. De Reuck aliongeza nguvu katika eneo la mwisho, huku Chama akiendelea kuonyesha kwa nini bado ana nafasi muhimu katika mfumo wa Simba.

Chama mwenyewe amekuwa kwenye moto katika mwanzo huu wa ligi, akiwa tayari amefikisha mabao manne. Umuhimu wake hauishii kwenye mabao; uwezo wake wa kutuliza mchezo, kufanya maamuzi na kutumia akili katika maeneo ya kushambulia unaifanya Simba iwe na mchezaji anayoweza kubadilisha mwelekeo wa mchezo.

Kilichoonekana zaidi leo ni namna Simba ilivyoweza kupata matokeo hata bila kutegemea kila kitu kutoka kwa mshambuliaji mmoja. Hilo linaifanya timu kuwa na sura pana zaidi ya kushambulia, huku wachezaji kama De Reuck na Chama wakionyesha kuwa hatari inaweza kuja kutoka maeneo tofauti ya uwanja.

Azam FC ilijaribu kuendelea kuwa ndani ya mchezo, lakini baada ya bao la kwanza Simba ilipata nafasi kubwa zaidi ya kudhibiti mwelekeo wa mchezo. Bao la pili likaja dakika tisa baadaye na kuzima matumaini ya wenyeji kurejea kwenye mchezo.

Mwisho wa Mzizima Derby, Simba imeondoka na pointi tatu na rekodi yake ya kutopoteza bado ipo hai. Ikiwa mwenendo huu utaendelea, swali la “Simba imejipata?” litaendelea kuwa moja ya mada kubwa katika mwanzo huu wa msimu, hasa kutokana na namna timu inavyoanza kuonyesha utambulisho wa mfumo wa Steve Barker. Ingawa ishara zinaonesha kocha ameanza kupata kikosi kinachoweza kutafsiri mbinu zake.

Comments