- Get link
- X
- Other Apps
Top Stories
- Get link
- X
- Other Apps
Mvutano kati ya Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu jezi mpya za Taifa Stars, umeanza kuibua maswali mazito zaidi ya biashara peke yake sasa unagusa suala la mipaka ya mamlaka ya Serikali katika uendeshaji wa soka nchini.
Katika tamko lake la Septemba 18, Sandaland imesema kauli ya Waziri iliyodai jezi hizo si za Taifa Stars imeigusa moja kwa moja heshima na biashara yake, ikikumbusha kuwa ina mkataba halali na TFF wa kutengeneza na kusambaza jezi hizo, ambazo tayari zimetumika katika mashindano kadhaa ya wanaume na wanawake. Kampuni hiyo imesema haitakaa kimya na imetangaza nia ya kwenda mahakamani.
Lakini zaidi ya mzozo wa kibiashara, sakata hili linaibua swali gumu zaidi je, Waziri wa Michezo ana mamlaka ya kisheria kuingilia mikataba na maamuzi ya kibiashara ya TFF?
Kwa mujibu wa mchambuzi wa muda mrefu wa soka, Jemedari Said, jibu ni hapana. Akitumia Kifungu cha 19 cha Katiba ya FIFA, Jemedari anaeleza kuwa kila shirikisho la soka duniani linatakiwa kuendesha mambo yake ikiwemo zabuni za wazalishaji wa vifaa vya michezo kama jezi bila kuingiliwa na mamlaka za nje, ikiwemo Serikali au Wizara husika.
Hatari, inaanza pale Serikali inapojaribu kubatilisha zabuni, kuvunja mkataba uliopo, au kulazimisha TFF kubadili mzabuni fulani. Hatua kama hizo zinaweza kutafsiriwa na FIFA kama kuingiliwa na mtu wa tatu jambo linalokiuka moja kwa moja kanuni ya uhuru wa mashirikisho.
Endapo hali hiyo itathibitika, FIFA ina uwezo wa kuchukua hatua kali dhidi ya nchi husika. Miongoni mwa adhabu zinazoweza kutolewa ni kusimamishwa kwa timu za taifa na klabu kushiriki mashindano ya kimataifa, ikiwemo michuano ya kufuzu Kombe la Dunia, pamoja na kusitishwa kwa ufadhili wa maendeleo unaotolewa na FIFA kwa shirikisho husika.
Katika hali mbaya zaidi, Jemedari anaeleza kuwa FIFA inaweza hata kuunda chombo maalum cha muda kusimamia shughuli za TFF, hadi hapo uhuru wa shirikisho utakaporejeshwa na ushawishi wa kisiasa kuondolewa kabisa.
Ni muhimu kufahamu kuwa maelezo ya Jemedari ni uchambuzi wa kanuni za FIFA na si tangazo kwamba FIFA tayari imechukua hatua dhidi ya Tanzania. Hata hivyo, kadiri mvutano kati ya Sandaland na Wizara unavyoendelea, ndivyo maswali kuhusu mipaka ya mamlaka ya Serikali katika masuala ya TFF yanavyozidi kupata uzito.

Comments
Post a Comment