Top Stories

Yanga yamsajili kiungo namba sita Fred Ngoma

Fred Ngoma akitambulishwa kiungo mpya wa Yanga SC


Yanga SC imemtambulisha kiungo wa kimataifa wa DR Congo, Fred Duval Ngoma, kama sehemu ya mipango ya kukiimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Usajili wa Ngoma umeelezwa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, kuwa unalenga kuziba pengo la kiungo namba sita ambalo klabu hiyo ilikuwa ikihitaji kulitatua baada ya kutofikia kiwango kilichotarajiwa katika majaribio yaliyopita.

Raisi wa Yanga Hersi Said amsajili Fred Ngoma


“Tumekosa huduma sahihi ya kiungo namba sita wa kiwango tulichokuwa tunakihitaji. Tumekuwa na kiu kubwa ya kuziba pengo hilo na tuna matumaini makubwa na ufanisi wa mchezaji ambaye tumemsajili,” alisema Hersi.

Ngoma, mwenye umri wa miaka 28, anacheza nafasi ya kiungo mkabaji na anafika Yanga akiwa na uzoefu wa kucheza katika ligi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Morocco, Libya na DR Congo.

Kwa mujibu wa takwimu za Transfermarkt, Ngoma amewahi kucheza michezo 84 katika mashindano mbalimbali akiwa amefunga mabao manne. Amehusika pia kwenye michuano ya CAF Confederation Cup, CAF Champions League na ligi za ndani za nchi alizowahi kucheza.

Mchezaji huyo aliyekuwa akicheza Olympique Safi ya Morocco kabla ya kujiunga na Yanga, ana thamani ya soko inayokadiriwa kuwa euro 450,000, huku nafasi yake kuu ikiwa ni kiungo wa ulinzi anayesaidia kuvunja mashambulizi na kusimamia eneo la kati la uwanja.

Usajili wa Ngoma unakuja wakati Yanga ikijiandaa na matukio muhimu kuelekea msimu mpya, ikiwemo Yanga Day inayotarajiwa kufanyika Agosti 9, siku ambayo klabu hiyo itawasilisha mipango yake kwa wanachama na mashabiki.

Baada ya Yanga Day, timu hiyo itaingia kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ngao ya Jamii dhidi ya mshindani wake, utakaochezwa katika Uwanja wa New Amani, Zanzibar, ikiwa sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa soka.

Comments