Top Stories

"Nitathibitisha ulikuwa sahihi... au nitakufa nikijaribu." Yan Diomande

Yan Diomande akisimulia safari yake kutoka Côte d'Ivoire hadi kutajwa kujiunga na Real Madrid.


Kuna nyakati ambazo mpira wa miguu huwa zaidi ya mchezo. Kwa Yan Diomande, kila dakika anayocheza uwanjani ni sehemu ya ahadi aliyomwekea dada yake, Roxane, ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 15.

Wakati nyota huyo wa Cote d'Ivoire akitajwa kuwa karibu kujiunga na Real Madrid katika dili linaloripotiwa kufikia euro milioni 120, simulizi yake imegusa mioyo ya mashabiki wengi duniani. Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo kuna safari ndefu ya kijana wa Afrika aliyekulia katika mazingira ya kawaida, lakini akiwa na ndoto zisizo za kawaida.

Yan alizaliwa na kukulia Abidjan, Cote d'Ivoire. Anakumbuka siku ambazo yeye na dada yake hawakujua maana ya utajiri au umaskini, bali walijua furaha pekee. Waliota siku moja kuondoka nyumbani, kuishi Ulaya na kubadilisha maisha ya familia yao.

"Unakumbuka mtu alinitengenezea jezi feki ya Manchester United, halafu nikandika 'Ronaldo 7' kwa kalamu nyeusi? Hatukujua utajiri wala umaskini. Tulijua furaha tu."

Anasema tangu akiwa mtoto, Roxane ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumuamini. Wakati wengine walikuwa wakiona ndoto zake ni kubwa kuliko uwezo wake, dada yake alimwambia siku moja angekuwa mchezaji mkubwa kuliko Cristiano Ronaldo.

Yan Diomande na dada yake Roxane ambaye alimhamasisha kufuata ndoto zake za soka.


Safari yake haikuwa rahisi. Akiwa na umri wa miaka tisa aliondoka nyumbani na kujiunga na akademi ya soka karibu na mpaka wa Ghana. Baadaye alihamia Marekani bila kujua hata neno moja la Kiingereza, akiamini ndoto yake ilikuwa inaanza kutimia.

Lakini badala ya mafanikio ya haraka, alikumbana na milango iliyofungwa.

Alifanya majaribio Bournemouth, Chelsea, Rangers, Olympiacos na Crystal Palace. Katika moja ya majaribio hayo, wachezaji Eberechi Eze na Michael Olise walimwambia alikuwa na kipaji kikubwa, lakini bado hakupata mkataba.

"Visa yangu iliisha. Ndoto yangu ikaonekana imefika mwisho. Walinirudisha Afrika, tukalia pamoja. Lakini wewe ndiye hukuacha kuniamini."

Baada ya kipindi hicho kigumu, Leganés wakampa nafasi mwaka 2025. Ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa ikaanza kutimia, huku mechi yake ya kwanza ikiwa dhidi ya Real Madrid.

Lakini furaha hiyo haikudumu.

Wiki chache baada ya kucheza mechi hiyo, alipokea simu iliyobadilisha maisha yake milele.

"Waliniambia tu, 'Dada yako ameondoka.' Nilishangaa. Nikasema, 'Unamaanisha nini?' Wakanijibu, 'Amefariki.' Roxane alikuwa na miaka 15 tu."

Yan amesema tangu siku hiyo maisha yake yalibadilika kabisa.

"Sihisi chochote tena. Ni kama mimi si binadamu. Tangu ulipofariki, nimekuwa mtupu."

Anasema hata hakulia siku alipopata taarifa hizo kwa sababu alikuwa katika mshtuko mkubwa.

Yan Diomande na dada yake Roxane ambaye alimhamasisha kufuata ndoto zake za soka.


Kupitia barua aliyomwandikia dada yake, Yan alieleza kuwa kila kitu anachokifanya uwanjani sasa kina lengo moja.

"Kila ninachofanya ndani ya uwanja ni kwa ajili yako. Nitahakikisha dunia nzima inalijua jina lako."

Anasema baada ya mechi yake ya kwanza dhidi ya Real Madrid aliweza hata kubadilishana jezi na Kylian Mbappé, jambo ambalo lilimkumbusha ndoto walizokuwa wakiziota pamoja walipokuwa watoto.

Lakini mafanikio hayo hayajambadilisha.

Yan amesema alipokuwa Leganés alikuwa akituma karibu fedha zote alizokuwa akilipwa nyumbani, huku yeye akiishi kwenye kituo cha mazoezi katika chumba kisicho na hata televisheni.

"Sikutaka nyumba kubwa. Sikutaka magari. Nilitaka kuweka kila kitu kwenye mpira wa miguu."

Anasema uwanja wa mpira ndiyo sehemu pekee inayompa utulivu kwa sababu anaamini ndipo anapoweza kuzungumza na dada yake.

Mwishoni mwa barua yake, Yan aliandika maneno ambayo leo yamekuwa alama ya safari yake ya maisha.

"Ulisema siku zote ningeweza kuwa bora kuliko Cristiano. Nitathibitisha ulikuwa sahihi... au nitakufa nikijaribu."

Yan Diomande katika safari ya soka


Wakati dunia ikisubiri kuona hatua yake inayofuata kuelekea Real Madrid, simulizi ya Yan Diomande imekuwa zaidi ya habari ya usajili. Ni simulizi ya matumaini, uvumilivu na ahadi ambayo kijana mmoja wa Afrika aliitoa kwa dada yake, ahadi ambayo anaendelea kuitimiza kila anapoingia uwanjani.

Comments